SIKU hizi ugomvi kwenye mahusiano imekuwa kama ni jambo la kawaida. Watu wanagombana kwelikweli. Utakuta mtu haipiti mwezi mmoja bila kugombana na mpenzi wake. Anampenda, hayupo tayari kumpoteza lakini maisha yao kila siku ni ugomvi. Mara nyingi ugomvi unapotokea, ladha ya pendo hupungua.Inachukua muda kurudi kwenye upendo wa awali mara baada ya wapendanao kugombana. Wahusika wanakuwa wanaukataa ugomvi lakini wapi, baada ya muda unatokea. Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wasomaji kuhusu suala zima la ugomvi.Ngoja ‘tushee’ hapa kwa pamoja ujumbe huu kutoka kwa dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Sasha: “Kaka naomba msaada wako, nimekuwa nikigombana mara kwa mara na mpenzi wangu. Imefika mahali hadi napoteza kabisa hamu ya mapenzi. Hata ninapotaka kukutana naye, nawaza tu lazima kutatokea ugomvi.“Wakati mwingine naamua kumuepuka kwa kutokutana naye au kutomsemesha kabisa. Napata furaha ninapokuwa peke yangu kuliko ninapokuwa na mpenzi wangu, inafika mahali mpaka nawaza niachane naye au vipi, naomba nisaidie kaka.”NINI CHA KUFANYA?Unapokutana na hali kama hiyo, unapaswa kutulia na kufanya maamuzi sahihi. Usikurupuke. Jiulize ni nini hasa kinachosababisha mgombane? Sema vizuri na moyo wako. Usijipendelee, kama unaona kuna kitu kinachosababisha mgombane na wewe ndio chanzo unapaswa kukishughulikia.Kama unaona kuna kitu mwenzako anakikosea, tafuta muda ambao mpo kwenye furaha na uzungumze naye kwa lugha rafiki. Muoneshe kwamba haipendezi mnapokuwa mnagombana mara kwa mara. Mueleze kwamba mnapofanya hivyo penzi lenu linapoteza msisimko. Mueleze kwamba ni hatari kuishi katika malumbano maana ni rahisi kujikuta mmeachana. Mfahamishe kwamba kama wote lengo lenu ni moja, kufika mbali kimahusiano kuna sababu gani ya kulumbana kila siku? Mnagombea nini?

CHUKULIANENI

Hili ndio somo muhimu katika mazungumzo yenu. Mueleze kwamba ili muweze kuishi vizuri mnapaswa kuchukuliana upungufu. Nyinyi mmekutana ukubwani. Kila mtu amelelewa katika maadili tofauti. Amekulia katika mazingira tofauti na mkaungana kutengeneza umoja wenu. Mnapaswa kuzungumza lugha moja. Kila mmoja amsome mwenzake kwamba nini anapenda na nini hapendi. Kitu gani huwa kinamuudhi mwenzako? Ukishakijua, epuka kumfanyia maana umeshajua hiyo ndiyo sababu ya nyinyi kugombana.

VUMILIANENENI

Kutokana na kila mtu kuwa na tabia na hulka zake, mnapaswa kuvumilia. Inawezekana kabisa mwenzako akawa na tabia flani ambayo kimsingi si njema lakini unachotakiwa kufanya ni kuibeba. Ishi naye kwa kuirekebisha taratibu. Tumia mbinu za kuzaliwa kumfanya abadilike. Mathalani, unaweza kumchukulia filamu yenye mafunzo kuhusiana na tabia yake na kumuwekea bila kujua kama umemfanyia makusudi. Unaweza pia kumpa majarida mbalimbali au magazeti yenye ujumbe unaohusu tabia yake naye akajifunza.

MFANYE AWE RAFIKI

Kumfanya mpenzi wako awe rafiki yako kutakufanya ujue mpenzi wako anapenda nini na nini hapendi. Hakikisha unakuwa naye karibu, mnazungumza kama marafiki hivyo kukupa mwanya mzuri wa kumuelewa vitu ambavyo huwa havipendi. Unapomweka karibu, anaweza kuwa anakusimulia juu ya mtu flani ambaye amemkwaza labda kwa kumfanyia jambo flani, ni rahisi na wewe kugundua kwamba hapendi kufanyiwa jambo hilo, ukaepukana nalo.

KUVUMILIANA KUNA KIWANGO

Fanya hayo yote lakini ukiona mnashindwa kabisa kuendana tabia na kila siku mnaendelea kugombana basi ni bora ukajiengua katika uhusiano huo. Utampata ambaye mnaendana. Vumilia katika kipindi flani, mbadilishe pale inapobidi kwa kutumia mbinu mbalimbali lakini mwisho wa siku ukiona haiwezekani, achana naye.
Give Your Comment
 
Top